Umuhimu wa Ujuzi wa Mawasiliano na Mahusiano katika Kupata Ajira na Kusimamia Biashara hasa kwa Wanafunzi Wanaomaliza Vyuo

Wahitimu wa vyuo wamemaliza mitihani na hivyo wameingia sokoni rasmi kutafuta ajira au kuanzisha biashara, na katika yote hayo kuna umuhimu mkubwa kwenye kuwa na ujuzi thabiti wa mawasiliano.

Nimegusia zaidi mawasiliano kwasababu ya historia yangu mwenyewe. Nilibahatika kusoma masomo yanayokuza uwezo na ujuzi wa mawasiliano kuanzia ngazi za chini; masomo ya lugha na kufikia chuo ambapo nilisoma Shahada ya Mahusiano kwa Umma na Utangazaji. Hata baada ya Shahada yangu, ninaendelea kuchukua kozi mbalimbali fupi na ndefu zinazosaidia kukuza ujuzi wangu wa kuwasiliana. Hata kampuni ya Serengeti Bytes ambayo mimi ni mwanzilishi mwenza nayo imejikita hukohuko, kutoa huduma za kitaalamu za mawasiliano kwa watu binafsi, makampuni, mashirika na kadhalika.Tuachane na hayo kidogo na tuangalie kwanini ujuzi wa mawasiliano ni muhimu sana kwa soko la ajira duniani kote.

Awali, uwezo na ujuzi wa kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa ufasaha ni muhimu sana kwenye ulimwengu wa biashara na ajira. Kwa msisitizo, uwezo wa kuwasiliana kwa ufasaha hasa kwa wanafunzi waliohitimu na wanaotafuta ajira ni muhimu, na hasa uwezo wa kuzungumza na kusikiliza. Na katika msingi huohuo, ujuzi wa mawasiliano si ujuzi ambao ni kitu kimoja, bali mjumuisho wa seti ya juzi kadhaa ambazo zikiwekwa pamoja zinakuwa na matokeo fulani yanayotarajiwa.

Kama mwajiriwa mtarajiwa, utapaswa kuwa na uwezo wa kujeleza kwa ufasaha na wakati mwingine kwa kifupi ili kuwavutia waajiri, lakini pia unapaswa kuwa msikilizaji mzuri na unayejua kuuliza maswali ya msingi. Mambo muhimu ya kuzingatia;
 • Ujuzi wa mawasiliano si tu kujua cha kusema, bali pia namna ya kusema na jinsi unavyojieleza (kujiwasilisha).
 • Kujua uchaguzi wa maneno sahihi ya kuuliza maswali ni ujuzi muhimu
 • Kutosema mengi pia ni ujuzi mzuri wa mawasiliano
 • Kufahamu hadhira yako na kufahamu nini cha kusema ni ujuzi mwingine muhimu wa mawasiliano kwa wahitimu wanaotafuta ajira
Ujuzi wa kina wa mawasiliano ni msingi wa ujuzi wa aina nyingine nyingi unaohitajika makazini na hata kwenye biashara. Mfano;
 • Uongozi na Utawala
 • Ushirikiano wa timu na kujenga mahusiano
 • Mawasiliano na wateja
 • Ujuzi wa Ushawishi
Mwanafunzi anapokuwa chuoni na hata nje ya chuo, kuna fursa nyingi za kuweza kuendeleza ujuzi wa mawasiliano ambao ni muhimu katika ajira na biashara. Fursa kama vile kufanya kazi sehemu zinazohusisha wateja, ajira kwenye usimamizi wa mitandao ya kijamii, uongozi ndani ya chuo na kadhalika ni muhimu kwenye kujenga uwezo.

Lakini pia, hata kwa wale ambao wapo nje ya sehemu kama hizo, wanaweza kukuza ujuzi wao wa mawasiliano kwa kuangalia uwasilishaji wa wazungumzaji maarufu kama wa kwenye TED Talks na kujifunza mbinu wanazotumia na kuchukua kozi mbalimbali fupi, za bure na za kulipia kutoka taasisi za elimu.

Vilevile, kama muhitimu ni muhimu kujifunza ujuzi wa kuandika kuanzia katika mazingira na matendo ya kila siku. Mfano, anza kuwasiliana na watu wako wa karibu kwa kutumia lugha rasmi ya Kiswahili au Kingereza. Epuka kuandika maneno kwa vifupisho ambavyo si rasmi hasa kwa kuwa watu wengi hukuchukulia kuwa si mtu ambaye anazingatia masuala.

Waajiri huwezaje kufanya tathmini ya ujuzi na uwezo wa mwajiriwa mtarajiwa ili kufanya uamuzi wa kumuajiri au kumuacha? Huangalia yafuatayo;
 • Kile unachoandika kwenye CV, Barua na Fomu ya Maombi ya ajira.
 • Jinsi unavyojibu maswali ya usahili.
 • Jinsi unavyojibu maswali ya usahili hasa yale yanayohusiana na ujuzi wako wa mawasiliano.
 • Uwezo unaoonesha kwenye usahili kwa njia ya maandishi.
 • Uwezo unaoonesha kwenye uwasilishaji mada.
 • Jinsi unavyoshirikiana na wenzako katika eneo la usahili, iwe ni katika makundi na shughuli rasmi za usahili au hata kwenye mazungumzo ya kijamii

Kulingana na mahitaji ya mwajiri, anaweza kuweka uzito kwenye umuhimu wa ujuzi wa mawasiliano na wapo watakaokushangaza kwa kiwango cha uhitaji wao. Ni muhimu kuhakikisha kuwa unaendelea na kuwa na utaratibu endelevu wa kujifunza namna bora zaidi ya kuwasiliana na hadhira na wadau wako.